Akizungumza na Nipashe mjini hapa jana, Kombo alisema ameamua kuchukua uamuzi huo kutokana na viongozi wa juu wa Chama Tanzania bara kushindwa kuheshimu uamuzi wa viongozi wa Zanzibar wa kususia uchaguzi huo.
Alisema viongozi wa Zanzibar wana haki ya kukaa, kujadili na kuamua mambo yanayohusu Zanzibar ikiwamo kushiriki au kutoshiriki uchaguzi wa marudio, jambo ambalo viongozi wa kitaifa wameshindwa kuheshimu hayo.
Kombo alisema Januari 31 na Febuari 2, mwaka huu, uongozi wa DP Zanzibar ulikutana na kujadili ajenda ya mkwamo wa uchaguzi na kukubaliana kutoshiriki uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika Machi 20, mwaka huu.
Alisema uongozi wa DP ukiongozwa na Katibu Mkuu Georgina Mtikila, umepinga uamuzi uliofikiwa na kuwasimamisha viongozi wa Zanzibar akiwamo Makamu Mwenyekiti, Peter Magwira, na Naibu wake Ramla Faki.
“Mie si Mgombea tena wa urais wa Zanzibar. Nimeamua kujivua uanachama wangu DP kutokana na kitendo kilichofanywa na viongozi wangu kupinga chama kususia uchaguzi wa marudio Zanzibar,” alisema Kombo.
Alisema uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana, ulikuwa huru na wa haki na hakuna sababu za msingi za kufanyika uchaguzi wa marudio.
Naye Magwira alithibitisha kuwa amesimamishwa uongozi pamoja na Faki. Alisema wamepokea barua ya Katibu Mkuu wa DP Febuari 5, mwaka huu, wakifahamishwa kusimamishwa kwao.
TADEA yakubali, Jahazi hapana
Katika hatua nyingine, uchaguzi huo wa marudio umeanza kuwa kizungumkuti baada ya chama cha Tadea kimepitisha azimio la kushiriki huku Jahazi Asili ikiwasilisha barua ya kususia.
Msimamo huo umetangzwa na Katibu Mwenezi wa Tadea Taifa, Rashid Mshenga baada ya kukamilika kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho kilichofanyika Magomeni Kondoa, Dar es salaam jana.
Alisema kikao hicho, chini ya Mwenyekiti Liffa Chipaka, kimepitisha kwa kauli moja chama kushiriki uchaguzi wa marudio.
Alisema wameamua kushiriki uchaguzi huo kwa sababu unafanyika kwa kuzingatia matakwa ya Katiba na sheria ya uchaguzi ya Zanzibar.
Katika uchaguzi uliofutwa matokeo na Mwenyekiti wake, Jecha Salim Jecha, kilimsimamisha Juma Ali Khatib kugombea nafasi hiyo.
Wakati huo huo, mgombea wa urais kupitia Jahazi Asilia, Kassim Bakar Ali, alisema jana mjini hapa kuwa amewasilisha rasmi barua Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) juu ya chama chake kutoshiriki uchaguzi wa marudio.
Alisema kimsingi uchaguzi ulishafanyika hivyo hawaooni sababu ya kuitishwa uchaguzi mpya na badala yake wakamilishe uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana.
Alisema kuwa azimio lake limepata baraka zote za chama na kuitaka ZEC kutotumia picha za wagombea wa chama hicho katika karatasi za wapigakura, ikiwamo nafasi ya urais.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa ZEC, Salum Kassim Ali, alisema anajiandaa kutoa taarifa rasmi juu ya vyama vilivyoamua kutoshiriki uchaguzi huo.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment