Kichanga Chaliwa na Mbwa Jijini Dar

Wananchi wa Kunduchi Mtongani, jijini Dar es salaam wameokota mwili wa mtoto mchanga aliyenyofolewa kichwa kwa kuliwa na mbwa.
Mmoja wa shuhuda wa tukio hilo, Thomas John aliliambia MTANZANIA kwamba wananchi walikibaini kichanga hicho baada ya kuburuzwa na mbwa kutoka kichakani kilikokuwa kimetupwa.

“Mtoto mchanga naona amezaliwa alfajiri ya leo (jana) na kutelekezwa na mama yake ambaye hadi muda huu wa saa 11 jioni bado hatujamtambua.

“Hili linaonekana sasa kuwa tatizo sugu kwa wanawake wenye roho za kinyama. Leo binadamu analiwa na mbwa kweli jamani Mungu wangu dunia yetu hii tunakwenda wapi,” alisema kwa masikitiko John

Alisema baada ya kubainika kwa mwili wa kichanga hicho walitoa taarifa kwa Mjumbe wa Nyumba Kumi ambaye aliwasiliana na polisi ili waje kwa ajili ya hatua za uchunguzi, lakini hadi kufikia saa 12 jioni hakuna askari aliyefika katika eneo hilo.
Mkazi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Hussein Juma alisema kwamba iwapo tukio hilo litaachwa bila kufanyika kwa uchunguzi wa kumpata muhusika upo uwezekano mkubwa kwa wanawake kuendelea kutupa watoto.

Alipoulizwa kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, alisema hana taarifa hizo, huku akiahidi kufutilia tukio hilo kwa ajili ya uchungu wa kina.

“Kwa kifupi sijapata taarifa hizo ndiyo kwanza unanipatia ila Jeshi la Polisi litafuatilia kwa karibu na likifanikiwa kumpata mtuhumiwa wa tukio hilo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake na tutatoa taarifa kwa umma,” alisema Kamanda Wambura.
Share on Google Plus

About Anonymous

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment