Binafsi namshukuru Mungu. Anaendelea kunibariki, amenipa uzima na kuniongoza katika hili pia. Niwaandikie hii barua ili kama tutaelewana, mwaka huu uwe na mabadiliko makubwa sana kwenu.
Dhumuni langu ni kutaka kuwakumbusha kuwa uigizaji hauishii ndani ya mipaka ya Tanzania. Mmeshuhudia Mtanzania anayeichezea klabu ya TP Mazembe, Mbwana Samatta. Ameliletea taifa letu heshima.
Ametwaa Tuzo ya Mwanasoka Bora wa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani.
Ni jambo la kujivunia maana anaweza sasa kwenda ‘duniani’, kushindana na mabara mengine na akaibuka kidedea. Hakuna kinachoshindikana chini ya jua.
Ndugu zangu, kutokana na kazi yangu, mimi ni mdau mzuri wa sanaa yenu. Mnapofanya vizuri natambua na mkiboronga najua. Kwa kipindi kirefu sasa mmekuwa mkifanya vizuri lakini zaidi ni ndani na si nje ya mipaka.
Sioni zile jitihada za makusudi za kuvuka mipaka. Sioni jitihada binafsi za mtu mmojammoja kuweza kupenya mipaka ya Kimataifa. Miaka mitatu kama si minne iliyopita, tasnia ya filamu ilikuwa na msisimko. Ushindani ulikuwa mkali kwa msanii na msanii.
Kolabo zenu na wasanii wa Nigeria zilianza kuleta matunda makubwa sana kwenye sanaa. Ule ulikuwa ndiyo mwanzo wa nyinyi kujitangaza, sasa zile harakati ziliishia wapi? Kwa nini msiziendeleze? Vyombo vya habari haviripoti kwa kiwango kikubwa habari zenu, lifanyieni kazi hilo.
Msikubali kuona wenzenu wa Bongo Fleva wanawakimbiza kila siku. Mwaka ndiyo kwanza unaanza. Wekeni mikakati thabiti kwa kuhakikisha mnafanya kazi bora. Kama kuna upungufu katika upande wa vifaa, hakikisheni mnapata vifaa vyenye ubora ndipo muigize.
Tena jitangazeni zaidi kwenye magazeti ya Global Publishers ambayo yanawafikia watu wengi nchini. Tovuti yetu inasomwa ulimwenguni kote. Unapotoka gazetini, habari yako inawafikia watu wote ulimwenguni kupitia tovuti.
Hapa ndipo mahala sahihi pa nyinyi kujitangaza. Msiwakimbie waandishi. Fanyeni kazi nzuri, watafuteni ili waweze kuripoti habari zenu. Huu si muda wa kuleta lawama. Bahati nzuri Waziri mwenye dhamana, Nape Nnauye ameonesha mikakati mizito ya kuwasaidia, basi msimuangushe.
Kasi ya rais wetu, Dk John Pombe Magufuli ameonesha njia ya kuchapakazi, kila mmoja wetu aoneshe kwa vitendo. Tumuunge mkono na tupate maisha mazuri kupitia kazi zenu.
0 comments:
Post a Comment