Na Victor Bariety, Geita
WATU watatu
wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita kwa tuhuma za kutaka
kuilipua hoteli moja maarufu iliyopo mjini hapa, Uwazi limefuatilia.
Akizungumza na gazeti hili wiki iliyopita, meneja wa hoteli hiyo, Chacha Wambura alisema tukio hilo lilipangwa kutekelezwa Novemba 3 na 4, mwaka huu. Meneja huyo alisema, awali kulikuwepo kwa taarifa za vitisho alizotumiwa mmiliki wa hoteli hiyo kati ya Oktoba 29 na 30, mwaka huu.
Alisema, yeye alipokea taarifa kutoka kwa bosi wake huyo akimtaarifu kuhusu kutumiwa meseji za vitisho kutoka kwa mtu asiyemjua, akimtaka amtumie pesa na asipotekeleza maelekezo hayo, angeilipua hoteli hiyo.
Meneja huyo alisema moja ya SMS hizo ilisomeka hivi: “Mimi siyo mtu mbaya kwako kwani ulishawahi kunikopesha pesa wakati ukiwa meneja wa benki ila kuna mfanyabiashara mmoja ndiye mbaya wako. Mimi nataka unitumie pesa.”
Wambura akaendelea kusema: “Binafsi nilishtuka baada ya kusikia taarifa hiyo. Nlichofanya, niliomba mlinzi wa pili kutoka kampuni ya ulinzi ya Kabasa Security na kutoa taarifa kwa jeshi la polisi.”
Aliongeza kuwa, Novemba Mosi mwaka huu, aliendelea kuchukua tahadhari akisaidiwa na askari wa upelelezi waliofanya uchunguzi maeneo yote ya hoteli hiyo na kuangalia kamera za usalama (CCTV) kama zinaonesha kuwepo kwa watu wanaoweza kutegesha vitu hotelini hapo lakini bila mafanikio.
Hata hivyo, alisema usiku saa 6:30, Novemba 4, mwaka huu, jeshi la polisi lilifanikiwa kumkamata mtuhumiwa David akiwa nje ya geti la kuingilia hotelini akiwa anachati na bosi wa Wambura akiendelea kumtaka atume pesa.
“Wakati polisi wanamkamata sikuwepo, ila walifanikiwa kwa sababu walimtaka bosi wangu aendelee kuchati na mtu huyo huku wao wakimfuatilia kwenye mtandao kujua mawasiliano yanatokea wapi,” alisema Wambura.
Wambura alisema aliiona meseji ya mwisho kutumiwa bosi wake ikisomeka: ”Naona umepuuzia ombi langu kwa sasa sitakusemesha tena ila tegemea hasara.”
Wambura akasema: “Kwa kweli hatujui sababu za kutaka kulipua hoteli kwa sababu hatumjui mbaya wetu hata huyo mtuhumiwa mimi sijamuona wala bosi wangu hajamuona kwa sababu polisi walituzuia.”
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, ACP Peter Kakamba alikiri kutokea kwa tukio hilo akiwataja watuhumiwa hao kuwa ni David Paulini (33), fundi wa kompyuta na mkazi wa Geita, Nelson Emmanuel Machimu (29), mlinzi wa kampuni moja ya mawasiliano mjini Geita na mtuhumiwa mwingine ni Alex Lituhungala (28), mkazi wa Kahama, Shinyanga ambaye pia ana makazi Babati mkoani Manyara.
Akibainisha sababu za kutaka kulipuliwa kwa hoteli hiyo, Kamanda Kakamba alisema watuhumiwa hao walitaka kufanya hivyo kwa lengo la kujipatia pesa kutoka kwa mmiliki wa hoteli hiyo.
Aliongeza kuwa, baada ya kumnasa David, polisi walikwenda kufanya upekuzi nyumbani kwake ambapo walimkuta na laini 3 za kampuni moja ya mtandao wa simu za mkononi, milipuko 10 na vilipuzi vyake huku milipuko mingine 8 ikikutwa Babati nyumbani kwa Alex.
0 comments:
Post a Comment