KASSIM
Kayira, anaendelea kusimulia maisha yake. Wiki iliyopita aliishia pale
alipotoa mfano wa kuku kutoka asubuhi kusaka chakula na kurudi jioni,
aliutoa mfano huo akiwa na maana kwamba, ukijua una uwezo fulani kikazi,
haihitaji kutumia nguvu nyingi kuuonesha.
HAPA ANAENDELEA…
“Niliendelea kufanya kazi katika Redio Idhaa ya Kinyarwanda. Nikafanya kwa muda kama wa miaka miwili hivi. Baadaye nikahamishiwa katika Idhaa ya Kiingereza. Nikaanza kufanya kipindi cha Focus of Africa,” anasema Kayira huku akinitazama kama mtu anayetaka nimuulize swali.
“Enhe ukaendelea na hicho kipindi kwa muda gani?” nilimuuliza.
“Hapo nilipiga kazi kwelikweli. Unajua siri ya mafanikio yangu mimi ni kujituma. Huwezi amini, nikiwa mfanyakazi wa Redio BBC, niliweza kupata tuzo mbalimbali chini ya wafanyakazi zaidi ya elfu 39 wa BBC duniani kote,” alisema Kayira kwa kujiamini.
“Tuzo gani hizo kaka ulizopata?” nilimuuliza huku nikimtazama usoni.
“Nilikuwa Mwandishi Bora na Mtaalam wa Lugha, Mfanyakazi Mwenye Nidhamu na Kujituma. Nilichapa kazi pale kwa takriban miaka 10. Baadaye nikaenda Makha kuhiji. Nikiwa huko sikuwa na mpango wa kurudi tena BBC lakini Salim Kikeke alimshawishi Mhariri Mwandamizi wa Televisheni ya BBC ili nirudi kwa upande huo.
“Niliridhia, nikarudi na kuanza kuripoti. Nikafanya ripoti nyingi ambazo zilinipa heshima nikawa natumwa nchi tofauti kuripoti,” anasema Kayira.
“Unakumbuka tukio gani katika kazi hiyo ya kuripoti?” nilimtwanga swali harakaharaka kabla hajaendelea.
“Matukio ni mengi lakini sitasahau niliwahi kwenda nchini Kongo kuripoti machafuko, tukarekodi siri za waasi wa serikali ambao walitushtukia. Wakatufuata hotelini, wakatunyang’anya vitu vyote, kuanzia kamera, fedha na bastola yangu.
“Sikukata tamaa. Nikaendelea kuripoti na baadaye nikarejea London , Makao Makuu ya BBC. Kazi zikaendelea,” anasena Kayira.
“Tukio gani ambalo huwezi kulisahau pale BBC?” nilimuuliza huku nikikaa vizuri na kutega sikio.
“Hahaha yapo matukio makubwa lakini sitasahau tukio moja la mimi kugombana na Kikeke. Tulikuwa mgahawani, mimi, Charles Hilal, Zuhura Yunus na Alex Murdhi. Kikeke akaja na fujo zake kwenye kibaiskeli, nikamwambia aache utoto, kama masihara tukagombana kweli pale lakini bahati nzuri niliongozwa na imani yangu, yakaisha tukaendele na shughuli zetu za kila siku,” anasema Kayira huku akijifuta jasho kidogo.
“Ulikaa kwa muda gani kwa mara nyingine BBC?” nilimuuliza.
“Nilikaa sana lakini baadaye nikaomba likizo ya muda mrefu. Nikarudi zangu nyumbani Uganda. Baadaye wakaniita tena, sikutaka kurudi lakini walinibembeleza, nikarudi tena kufanya kazi hadi mkataba wangu wa miaka mitatu ulipoisha mwaka jana,” alisema Kayira na kuongeza:
“Hapo ndipo niliposema sitaki tena kazi ya utangazaji, nikalipwa kiinua mgongo kama shilingi Mil. 280 za Kitanzania. Hapo akili yangu yote ikawa kwenye kuwekeza katika biashara zangu Uganda,” alisema huku akijiandaa kuagana na mimi.
“Sasa kaka hujaniambia maisha baada ya hapo nini kilifuata hujaniambia hata maisha yako ukiwa nyumbani inakuwaje?” nilimuuliza kabla hajainuka.
“Maisha ya nyumbani mimi napenda kupika. Unajua mimi nilikuwa baba ntilie kipindi cha nyuma wakati maisha yalipokuwa magumu. Nilijua sana kupika hivyo napenda sana kazi hiyo.
“By the way, baada ya kusema naachana na utangazaji, nilipokea simu kutoka kwa Tiddo Mhando wa Azam TV, Tanzania. Akaniomba nije kufanya mazungumzo ya kazi, nilikataa, nikamwambia mimi sitaki tena kazi ya utangazaji.
“Akanibembeleza nije Tanzania kumsikiliza. Nikaona nije kumsikiliza, wakanishwishi nikawe Mkurugenzi Mtendaji wa Azam Tawi la Uganda nyumbani kwetu.
“Wakanipa ofa ya mshahara wa shilingi Mil. 18 za Kitanzania, nyumba na gari la kutembelea aina ya Toyota Land Cruiser GX V8, sasa ndiyo nakamilisha taratibu za ofa hizo, narudi nyumbani Uganda kufanya kazi hiyo pamoja na shughuli zangu za kijasiriamali.”
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment