Jakaya KIKWETE Amfungukia Mbwana SAMATTTA

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete amempongeza mwanasoka bora wa Afrika, Mbwana Samatta kwa mafanikio aliyopata na sasa amemtaka alenge kucheza ligi kubwa za Ulaya ili Watanzania waweze kumuona kila Jumamosi kupitia kwenye luninga.

Kikwete ambaye ni Rais mstaafu amesema tuzo ya Mwanasoka Bora wa Afrika aliyoipata itasaidia kutangaza soka ya Tanzania, kuwapa ari wachezaji wengine na kuwapa furaha Watanzania ambao wamekuwa na kiu ya kuona nchi inafanya vizuri zaidi.
“Angalau Mbwana ametuinua kwenye soka. Ametupa ari mpya. Ametupa furaha.

Binafsi nampongeza kwa mafanikio,” alisema Kikwete alipotembelewa na mwanasoka huyo jana kwenye ofisi za CCM, Lumumba, Dar es Salaam. “Narudia maneno niliyomuambia tulipokutana pale Kinshasa (DRC); alenge juu zaidi, shabaha iwe kucheza Ligi Kuu za Ulaya.

Tunapenda kila Jumamosi tukiangalia kwenye luninga tumuone Mbwana anatikisa nyavu, ni jambo la fahari, namtakia kila la kheri,” alisema Kikwete.

Kikwete hakusita kuonyesha furaha yake juu ya mafanikio hayo ya Mbwana na kusema Tanzania kwa muda mrefu imekosa furaha na imejawa na ukame wa makombe. “Baba yake alikuwa mwanamichezo, mshale umerudi kule kule,” alisema na kuongeza: “Waziri wa Michezo (alimgeukia Nape Nauye) naomba muangalie namna ya kumsaidia kijana huyu afike mbali zaidi.” Mbwana ambaye ni mchezaji wa klabu ya TP Mazembe ya DRC Alhamisi iliyopita alitwaa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa Wachezaji wa Barani Afrika katika hafla iliyoandaliwa Lagos, Nigeria.

Aidha, mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 24 amekuwa Mtanzania wa kwanza na mchezaji wa kwanza kutoka nchi za Afrika Mashariki kunyakua tuzo hiyo baada ya kuiongoza TP Mazembe kutwaa ubingwa wa Afrika yeye akipachika nyavuni mabao sita. Klabu kadhaa maarufu za nchi za Ulaya zinataka kumsajili, lakini tayari FC Genk ya Ubelgiji imekwishanasa saini yake.
Akizungumza katika ziara hiyo Mbwana alisema: “Siri kubwa ya ushindi ni nidhamu na kujituma. Lakini kubwa zaidi lililonipa changamoto ya kuhakikisha ninaongeza bidii zaidi kwenye kazi yangu ni pale nilipokutana na Rais mstaafu Jakaya Kikwete pale Kinshasa. Tulizungumza mambo mengi nikiwa na mwenzangu Thomas Ulimwengu, lakini kubwa alituasa tusikubali kubaki Afrika tujitahidi kwenda kucheza Ulaya.” “Nakumbuka Rais Kikwete alituambia maneno haya, tumeonyesha njia tusikubali kubakia Afrika tujitahidi kwenda kucheza Ulaya ili kuonyesha njia kwa vipaji vingine ambavyo viko nyumbani.

Alisema ninyi ndiyo alama ya mfano, Watanzania karibu wote tunawategemea kwenye medani ya soka. Mjitahidi msituangushe,” alisema.“Maneno haya kwa kiasi kikubwa yalinisukuma kuona ikiwa Rais anasema hivi, je familia yangu au watu wa karibu na sehemu niliyotokea wanachukuliaje hili suala, ilinipa ari na inabidi nifanye vizuri. Nashukuru Mungu amenisaidia,” aliongeza.

Alisema anaiweka tuzo hiyo kwa heshima ya Kikwete na kumuahidi kufika mbali zaidi. “Naomba baraka zake. Naomba Watanzania wazidi kuniombea,” alisema na kumkabidhi Kikwete jezi namba tisa yenye jina lake ‘Mbwana Samatta.
Share on Google Plus

About Anonymous

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment