HALI tete! Kufuatia Mahakama ya Ardhi, Dar kutengua bomoabomoa ya
nyumba 674, bado ripoti inatisha kwa zile nyumba ambazo mahakama
haikuzitambua na zile ambazo zilishabomolewa mwishoni mwa mwaka jana.
Moja ya mjengo wa ukibomolewa.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa wengi waliokimbilia
mahakamani, walikuwa wakisukumwa na baadhi ya vigogo wenye mahekalu yao
maeneo ya Mbezi, Dar ambao walikuwa wanashindwa kujitokeza mstari wa
mbele kwa kuhofia kuhojiwa au kujulikana nyumba zao ambazo walikuwa
wakizimiliki kwa siri.
Imebainika kuwa baadhi ya vigogo hao ni wale wanaofanya kazi
serikalini ambapo mijengo yao haifanani na mishahara wanayoipata hivyo
kuingia kwenye ‘figisufigisu’ ya uhujumu uchumi.
…….Tingatinga likifanya yake.
Wakati hali ikiwa hivyo, imebainika kuwa mfanyabiashara maarufu
jijini Dar, Muzamil Katunzi ni miongoni mwa watu ambao wamekumbwa na
sekeseke hilo baada ya kubomolewa uzio wa kiwanja chake kilichopo Mbezi
Beach.
Naye bosi wa Kampuni ya Udalali ya Majembe Auction Mart aliyejulikana
kwa jina moja la Mwamoto, anayemiliki nyumba eneo la Mbezi, yeye
ameamua kubomoa mwenyewe sehemu ya ukuta wa nyumba yake kabla ya
serikali kuingilia kati ili aweze kunusuru mali zake.
Hata
hivyo, katika hali isiyokuwa ya kawaida, mahekalu mengi ya watu
wanaodaiwa kuwa ni baadhi ya vigogo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),
hayajawekewa alama ya X ‘bomoa’ kufuatia kujengwa umbali wa mita 60
kutoka baharini ambapo ndiyo sheria inavyotaka.
Juzi, kwenye Mahakama ya Ardhi, korti ilisema inatambua nyumba 674 tu
zilizopo Wilaya ya Kinondoni, Dar ambazo zina pingamizi la kisheria.
Kwa
mujibu wa mahakama, kesi kuhusu pingamizi la nyumba hizo itatajwa
mahakamani Jumatatu, Januari 11, 2016. Nyumba hizo 674, mahakama imesema
hazitakiwi kuguswa na bomoabomoa kwa sababu upande wa serikali haujatoa
vibali vinavyotosheleza kuifanya mahakama iamuru zibomolewe.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, nyumba ambazo mahakama haikuzitambua,
serikali itaamua yenyewe inabomoa lini kulingana na utaratibu wake.
“Sasa hivi tunabomoa maeneo ya Mbuyuni na Hananasif, maeneo mengine
kama Mbezi Beach na kwingineko, tunasubiri maelekezo kutoka ngazi za
juu,” Arnold Kisiraga, Afisa Utunzaji wa Mazingira kutoka Baraza la
Taifa la Uhifadhi wa Mazingira (NEMC) aliliambia Amani.
Katika
uchunguzi wa gazeti hili, imebainika kwamba baadhi ya vigogo ambao
nyumba zao zipo kwenye mkumbo wa kubomolewa, wameshaanza kutafuta makazi
Uswahilini, wengine wanahamisha vyombo vyao wakikwepa kupata hasara.
“Wengi wanalia, wengine wamepata presha kwa vile baada ya bomoabomoa hawajui watakwenda wapi,” kilisema chanzo chetu.
Waandishi: Issa Mnally, Boniphace Ngumije, Chande Abdallah na Makongoro Oging’.
0 comments:
Post a Comment