Kocha wa Azam FC, Stewart Hall.
Martha Mboma,Dar es SalaamKOCHA wa Azam FC, Stewart Hall, ameonekana kuwa moto zaidi kwenye mechi za mikoani na kuwafunika Wazungu wenzake, Dylan Kerr wa Simba na Hans van Der Pluijm wa Yanga.
Azam ambayo imecheza mechi nne mkoani, imeonekana kuwa moto zaidi kwani imefanikiwa kushinda zote huku Yanga ikishinda tatu kati ya tano wakati Simba iliyo chini ya Muingereza Kerr ikitakata kwenye mechi tatu kati ya sita ilizocheza.
Azam yenyewe ilifanikiwa kushinda mechi dhidi ya Stand United ambayo iliichapa mabao 2-0 kisha ikairarua Mwadui 1-0 kabla ya kuipa kichapo kama hicho Ndanda FC ya Mtwara na kumalizia kwa Majimaji huko Songea kwa kuilambisha mabao 2-1.
Kwa matokeo hayo, Azam imefanikiwa kuvuna pointi 12 katika michezo minne iliyoshuka dimbani na kumfanya Stewart kuwakimbiza Wazungu wenzake Kerr na Pluijm kwenye michezo ya mikoani.
Baada ya hapo ikacheza na Kagera Sugar na kuichapa mabao 2-0, ikabanwa na Mgambo ya Tanga kwa kutofungana kisha ikaichapa African Sports ya mkoani humo bao 1-0, hivyo kujikusanyia pointi 11 mpaka sasa kutoka mikoani katika michezo mitano.
Simba yenyewe ilianza kwa kuvunja mwiko wa kutopata ushindi kwenye mechi za Mkwakwani mkoani Tanga kwa kuzifunga timu za African Sports bao 1-0, pia ikaichapa Mgambo 2-0 kisha ikasafiri hadi Mbeya na kuichapa Mbeya City bao 1-0 lakini ikapunguzwa kasi na Prisons kwa kuchapwa bao 1-0 kabla ya kubanwa mbavu na Toto ya Mwanza kwa kutoka nayo sare ya bao 1-1.
Katika mchezo wa juzi Jumamosi pia Simba ilibanwa mbavu na Mwadui ya Shinyanga na kutoka nayo sare ya bao 1-1 hivyo kutoka mikoani wakiwa na pointi 11 sawa na Yanga ambao wao wamecheza mechi tano pekee.
0 comments:
Post a Comment