Waziri
wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Nape Nnauye amesema
Watanzania wanapaswa kumuombea Rais John Magufuli ili aendelee kutumbua
majipu kwani nchi ilifika pagumu baada ya wezi kuonekana wajanja.
Akizungumza
wakati akizindua tamasha la Krismasi lililofanyika katika Ukumbi wa
Diamond Jubilee, Dar es Salaam Nape aliyemwakilisha Makamu wa Rais,
Samia Suluhu Hassan alisema haijalishi mafisadi nchini wamejenga mizizi
kiasi gani, lazima majipu yote yatumbuliwe.
Alisema
kila mmoja anatakiwa kuomba kwa imani yake kwani kazi aliyoifanya Rais
Magufuli na anayotarajia kuendelea kuifanya sambamba na Baraza la
Mawaziri na viongozi wengine ni kubwa.
Nape
alisema kazi ya kutumbua majipu siyo ndogo, kwani Dk Magufuli na jopo
lake wanaamini kwamba Watanzania wana haki ya kufaidi matunda ya nchi
yao.
''Nchi
ilifikia hatua ngumu asiyeiba alionekana mjinga na mshamba na wezi
walionekana wajanja, waliostaafu wakiwa maskini walionekana wajinga,
muombeni Rais Magufuli atumbue majipu ili Watanzania wafaidi matunda ya
nchi yao'', alisema Nape.
Alisema
hakuna sababu kwa nchi kuendelea kuwa maskini, mwenye haki atapata haki
yake huku kila mmoja akila kwa jasho lake na si vinginevyo.
Waziri huyo ambaye aliimba pambio liitwalo Yu Mwamba, alisema amani na utulivu wa nchi lazima viendelee na ili hayo yote yafanikiwe, Watanzania wanapaswa kuomba.
''Serikali
tutahakikisha tunaitunza amani kwa gharama yoyote, hivyo viongozi wa
Serikali na kidini wanapaswa kudumisha dhana hiyo ili nchi iendelee kuwa
kisiwa cha amani, yapo mataifa yanatamani kuwa kama Tanzania lakini
haiwezekani'', alisema Nape.
Nape
alizindua albamu ya kwaya ya Wakorintho wa Pili kutoka Mafinga, Iringa
na kuinunua kwa Sh1.5 milioni. Maaskofu na viongozi wa dini walifanya
sala kwa dakika 15 iliyokuwa na lengo la kumwombea Rais Magufuli ili
Mungu amlinde katika jitihada zake za kupambana na mafisadi.
Awali,
Askofu David Mwasota alisema viongozi wa dini wanaunga mkono Serikali
ya Awamu Tano kwa kutambua haki kwa Watanzania wote.
''Tunampongeza
Rais Magufuli kwa jitihada zake ambazo kwa muda mfupi amefanya mambo
makubwa yanayoonyesha nuru kwa nchi yetu miaka mitano ijayo'', alisema Askofu Mwasota.

0 comments:
Post a Comment