Alikuwa anataka kupeleka posa kwa binti mmoja ambaye ni kabila langu hivyo mimi nilitegemewa kuwa najua mila na taratibu za kutoa posa. Basi kama tulivyokuwa tumepangiwa na wakwe watarajiwa, juzi saa kumi jioni tukawasili kwa wakwe watarajiwa.
Tulichelewa kama dakika tano si unajua foleni tena, hiyo ikawa nongwa ya kwanza. Wajomba wakatuambia turudi wiki inayofuata tukajifunze namna ya kuwahi, tukaanza kuomba msamaha na kubembeleza, baada ya faini ya shilingi elfu ishirini tukaruhusiwa kusikilizwa.
Tulimkuta baba wa binti na wajomba wawili wanatusubiri, tukakaribishwa kwenye viti na kukaribishwa vinywaji. Tukaomba maji, unajua siku kama hii ukiomba bia kabla hawajapokea barua inaweza kuwa kisa cha kukataa kupokea barua, utasikia wanasema wakwe wenyewe walevi, kwa hiyo ni muhimu kuwa falafala kiasi.

Mwanaume nikaomba msamaha na kupiga magoti mbele ya baba mkwe. Kwa sauti ya unyonge nikaeleza kuwa tumemuona binti pale kwake na tulikuwa tunaomba kuleta barua ya kuunga ukoo. Nikaanza kusailiwa kuhusu muoaji, hali yake ya kimaisha na kadhalika.
Kwa kuwa jamaa yangu maarufu pale mtaani, ilikuwa rahisi kuwataarifu kuwa muoaji ni kijana mwenye uwezo wa kumtunza binti, tayari ana mjengo wa nguvu si mbali na pale na ana magari kadhaa mengine ya bei mbaya na kwa ujumla mtoto wao hatapata shida maishani.
Wale wazee wakatuomba tutoke nje wajadili kitu. Dakika chache baadae tukaitwa tena ndani. Mjomba mmoja wapo akaanza. “Umesema muoaji ndiye mwenye kaghorofa hapo bondeni?” Nikajibu ndiyo. “Na huyo muoaji si huyu mwenye lile gari jekundu lenye maspika yana kelele akipita hapa mtaani?” Nikatikisa kichwa kukubali maana jamaa yangu bishoo sana ndiyo zake hizo.
Maswali yakaendelea, “Hivi anafanya kazi wapi”? Nikawajibu mfanyabiashara. “Biashara gani”? Swali hili likawa gumu maana hata mimi sijawahi kujua jamaa anafanya biashara gani. Nikajibu sina uhakika. Hapo wale wazee wakaniambia;
“Rudi na barua yako. Lile ghorofa litabomolewa siku hizi hizi maana liko eneo la bonde la mto na kwa kuwa biashara ya ndugu yako haijulikani atatumbuliwa jipu siku hizihizi, unataka binti yetu aanze maisha kwa kumpelekea mumewe uji magereza? Ondokeni haraka hapa na kiposa chenu’ Daah!

0 comments:
Post a Comment