Za Chembe Lazima Ukae
Ojuku Abraham, +255 719 786 355
MIAKA kadhaa ya
kufanya kazi na watu wenye majina makubwa, wenye mamlaka na walio
katika nafasi nyeti, imenipatia funzo kwamba unapaswa kuwa makini sana
kwa nyendo zako, kama lengo lako ni kuwa mtu maarufu, lakini mwenye
hadhi katika jamii.
Unapokuwa mtu maarufu, unachukuliwa kama
mfano na bahati mbaya, mfano ni mfano tu, uwe mbaya au mzuri. Mtu
anaweza kumwambia mwanaye kwa mfano, asiwe malaya kama Kim Kardansian,
yule dada mrembo mwenye msururu wa wanaume aliotokanao huko Marekani. Ni
staa mkubwa lakini mwenye sifa mbaya, licha ya hivi sasa kuwa mke wa
Kanye West.
Na mtu mwingine anaweza kukuambia kuwa wapaswa kuwa na nidhamu, heshima na utu kama Ronaldo de Lima, mwanasoka nyota aliyepata kila aina ya mafanikio uwanjani, akishinda mataji yote makubwa ya soka duniani, lakini akibakia kuwa muungwana uwanjani, mpole nje ya uwanja na mwenye utu katika maisha ya kijamii.
Umaarufu unakufanya uwe mtu wa kutazamwa kwa kila unachokifanya. Watu wataulizana, hivi fulani ameoa? Ana watoto wangapi, maisha yake yakoje, anapendeleaga nini na mambo mengine chungu nzima. Na mara nyingi, umaarufu unapatikana kupitia kazi tunazofanya.
Lakini umaarufu huu nao umegawanyika, ule wa sifa mbaya na ule wenye hadhi. Tunao mastaa ambao siku zote tunategemea kusikia juu ya skendo na inapotokea wakatokea kwenye shughuli zenye heshima, kila mmoja huidharau hafla hiyo. Hawa wapo na wote tunawajua.
Lakini wapo baadhi ya mastaa wetu ambao inakuwa vigumu kidogo kuamini tunaposikia habari mbaya zinazowahusu, hata kama ni kweli wamefanya kinachosemwa. Hii ni kutokana na jinsi wao wenyewe walivyojitengeneza katika umaarufu wao.
Enzi zile nikikua, kulikuwa na jambazi mmoja maarufu sana jijini Dar es Salaam, akiitwa Nyau. Habari zake zilitingisha kila kona na kila mmoja aliogopa kukutana naye. Ziliposikika habari kwamba ameuawa, kila mpenda amani alifurahi. Unapoona watu wanafurahia anguko lako, ni dhahiri, maisha yako yalikinzana na matazamio yao!
Wapo watu wanaotafuta majina makubwa ili wafanye utapeli na umalaya. Lengo lao ni kutumia umaarufu wa majina yao ili kufanikisha lengo lake. Bahati mbaya inakuja pale anapoitumia fani kutimiza lengo lake, matokeo yake ni kuonekana watu wote walio katika industry kuwa ni wenye sifa kama zake.
“Unataka kuwa muigizaji, achana na hiyo fani, wasichana wa Bongo Movie ni malaya,” mtu mmoja anaweza kumwambia binti anayejaribu kupenyeza ili awe muigizaji, aweze kutimiza ndoto zake za muda mrefu.
Hii haimaanishi kweli kuwa Bongo Movie ni chaka la wahuni, isipokuwa kwa sababu mtu mmoja au wawili, wameitumia fani hiyo vibaya. Watu wengine wamejaribu kuwa wasanii wa Muziki wa Kizazi Kipya, dansi au taarab, wakiamini huko kunaweza kupata umaarufu.
Ninajua wapo wasanii wenye majina makubwa, lakini wanayatumia vizuri kuchangamkia fursa zinazokuja mbele yao, hawa sina tatizo nao. Lakini sipendezwi zaidi na matapeli au malaya wanaotumia fani kutekeleza matakwa yao.
Rai yangu ni kwa jamii zinazohusika, kuwakataa watu hawa kuwa miongoni mwao. Tusikubali matapeli wajineemeshe kwa majina wanayoyapata kupitia fani zetu. Uzuri ni kuwa tunajuana, tunafahamu kuwa huyu anaishi kwa sababu ya utapeli au wanaume, fani ni kigezo tu, tumkatae!
0 comments:
Post a Comment