Stori: Gabriel Ng’osha, Dar na Gregory Nyankaira, Mara
VILIO na majonzi vilitawala nyumbani kwa mzee Mfungo Mtaengelwa
wakati wa mazishi ya kijana wake, Mafwiri Mfungo, 28, aliyekuwa
mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), aliyeuawa kwa kupigwa
risasi tatu kifuani na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi. Tukio hilo
linalowaliza wanachuo wenzake mpaka sasa, lilijiri Desemba 15, mwaka
huu, Ubungo Msewe jijini Dar es Salaam.
Jeneza lenye mwili wa marehemu.
ALIYEKUWA NAYE ASIMULIA
Beatus Chrispian ambaye alikuwa rafiki mkubwa wa Mafwiri, wakiishi
nyumba moja na aliyekuwa na marehemu hadi dakika za mwisho, anasema yeye
alinusurika katika tukio hilo baada ya kujeruhiwa kwa risasi tumboni.
Beatus Chrispian aliyejeruhiwa.
Alisema: “Siku ya tukio tulikuwa ndani, saa 2 usiku, tukipanga mipango ya kesho yake. Ghafla tulisikia mlipuko mkubwa nje.
“Tulitoka nje na kuona cheche za moto zikitokea karibu na transfoma
moja ya umeme. Tukadhani huenda transfoma hiyo ilikuwa inalipuka,
tukaenda ili kushuhudia kama ni kweli tuwajulishe Tanesco.”
MAREHEMU ANASHIKILIA TUMBO
“Kabla hatujafika, ghafla nikamwona marehemu anainama na kushikilia
tumbo huku akilia kwa uchungu. Na mimi nikasikia kama kitu cha baridi
kimenichoma tumboni. Ilibidi nikimbilie ndani. Nikashangaa kuona damu
zinanitoka tumboni, nikagundua kumbe nilikuwa nimepigwa risasi. Muda
mfupi baadaye nikasikia vilio vya watu huku wakilitaja jina la Mafwiri…
Mafwiri. “Nilipojikaza na kwenda eneo hilo, nilimkuta Mafwiri amelala
chini, kumbe alishafariki dunia. Alikuwa na majeraha matatu ya risasi
kifuani.”
Kabuli la marehemu Mafwiri
KILICHOJULIKANA
Beatus alisema, baada ya tukio hilo ilibainika kuwa maduka matano,
likiwemo moja la pesa yalikuwa yameporwa fedha na majambazi hao.
“Inaonekana sisi tulipokwenda, walituona, wakajua tunawafuatilia
ndiyo maana wakatupiga risasi,” alisema Beatus akiwa na jeraha tumboni.
Marehemu Mafwiri wakati wa uhai wake, baada ya kuhitimu kidato cha
sita na kozi ya ufundi katika Chuo cha Ufundi Moshi, Kilimanjaro,
aliajiriwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) jijini Mwanza, 2009.
Mwaka 2012, alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akisomea shahada
ya uhandisi (Engineering) hadi alipofikwa na mauti. Pia alikuwa Naibu
Waziri wa Miundombinu katika serikali ya wanafunzi chuoni hapo.
Marehemu Mafwiri alizikwa Desemba 20, mwaka huu nyumbani kwao,
Kitongoji cha Sabasaba, Kijiji cha Nyamisisi, Wilaya ya Butiama mkoani
Mara. Ameacha watoto wawili.
….waombolezaji.
0 comments:
Post a Comment