Sababu Za Wanaume
Natumai mu wazima wa afya. Leo katika mada yangu hii, nataka kuzungumzia zaidi sababu za wanaume wengi kukosa hamu ya tendo la ndoa.
Kama ilivyo matatizo mengine, tatizo la
kukosa hamu ya kushiriki tendo la ndoa huwakumba na wanaume vilevile ila
siyo kwa kiwango kikubwa kama ilivyo kwa wanawake.
Katika makala haya, tutaangalia kwa kina sababu za tatizo hili kwa wanaume na athari zake.
Mwili wa mwanadamu uliumbwa na matamanio
na si mabaya kama mwenye mwili atakuwa na uwezo wa kujitawala. Wanaume
wengi huvutiwa zaidi na hisia za kushiriki tendo la ndoa kwa kuona
baadhi ya maungo kwa wanawake, kusikia sauti na hata migusano.
SIYO KUUTAWALA MWILI
Kuna wanaume ambao wapo tu, ilimradi
siku zinakwenda, hawapati hamu ya kushiriki tendo la ndoa na wanajiona
kama ndiyo wamefanikiwa kujitawala, kumbe ni wagonjwa.
Habari njema ni kwamba, licha ya tatizo
hilo kuwasumbua wengi, kuna mambo unayoweza kuyafanya kupunguza ukubwa
wa tatizo hili au kuliondoa kabisa kwa kutumia mimea tiba na matunda
tiba.
Unachotakiwa kufanya, kama umejaribu
kutumia njia mbalimbali kuondoa tatizo hili bila mafanikio, basi wahi
mapema kwa wataalamu ukafanyiwe uchunguzi.
Baadhi ya wanaume wanamini kuwa, hamu ya
kufanya tendo la ndoa inapungua kadiri umri wa mwanaume unavyoongezeka.
Kuna idadi kubwa ya wanaume ambao hamu yao ya kufanya tendo la ndoa
imebaki vilevile hata umri wao kuwa mkubwa.
UKUBWA WA TATIZO KATIKA JAMII
Kwanza tuanze kwa kutazama ukubwa wa
tatizo hili. Idadi ya wanaume wanaoridhika kuishi na tatizo hili ni
ndogo sana ukilinganisha na ile ya wanawake.
Hata hivyo, tatizo la wanaume kukosa
hamu ya kushiriki tendo la ndoa limekuwa ni chanzo kikubwa katika kuleta
migogoro katika familia.
Wanaume kwa kawaida ni wabishi na huwa
hawapendi kuaibika hivyo mtu anaweza akawa na tatizo lakini asipende
mwenza wake ajue kama analo ambapo kumbe kama angeliweka bayana angepata
ushauri wa namna ya kulitatua.
Pamoja na kwamba tatizo hili
halijitokezi sana kwa wanaume ukilinganisha na wanawake, inakadiriwa
kuwa asilimia 15 hadi 16 ya wanaume wana tatizo hili. Ni sawa na uwiano
wa mwanaume mmoja mwenye tatizo hili katika kila wanaume sita au saba.
Idadi ya wanawake wenye tatizo hili ni mara mbili ya wanaume.
WANAUME WANAKEREKA ZAIDI
Tatizo hili huwakera zaidi wanaume
kuliko wanawake kwa sababu wanaume huchukulia urijali kama sehemu ya
ukamilifu wa mwanaume na wanakosa raha wanapoona wana upungufu kuhusu
mambo ya mapenzi tofauti na wanawake.
SABABU AU CHANZO CHA TATIZO
Tatizo la kukosa hamu ya kufanya tendo la ndoa kwa wanaume linaweza kusababishwa na vitu vingi.
Sababu hizo zinaweza kuwa za kimaumbile,
kisaikolojia au za mchanganyiko wa vitu hivyo viwili. Hebu tuone baadhi
ya vyanzo vya tatizo hili.
UHUSIANO BAINA YA MWANAUME NA MWANAMKE
Uhusiano kati ya mwanaume na mwanamke ambao ni wanandoa una mchango mkubwa katika kujenga au kubomoa matamanio ya mwanaume.
Kama kutakuwa na matatizo ya uhusiano
kama vile ugomvi kati ya wawili hao, kuna mchango mkubwa katika
kusababisha tatizo la mwanaume kukosa hamu ya tendo la ndoa.
Ni vyema ukajihoji kama uhusiano wako na mwenza wako upo sawasawa.
MAZOEA
Mara nyingine mwanaume anaweza akawa
katika uhusiano kwa muda mrefu kiasi ambacho amemzoea mwanamke hali
inayosababisha mwanaume huyo kukosa hamu ya kushiriki tendo la ndoa.
Hili nalo hutokea mara nyingi.
MATUMIZI YA MADAWA YA KULEVYA
Matumizi ya baadhi ya madawa na unywaji
wa pombe wa kupindukia huweza kuleta tatizo hili la mwanaume kukosa hamu
ya kufanya tendo la ndoa. Madawa yanayochangia tatizo hili ni ya High
blood pressure, ya kuondoa msongo wa mawazo, yote yanayozuia ufanyaji
kazi au uzalishaji wa Testosterone. Mfano, Cimetidine, Finasteride
na Cyproterone.
MATATIZO KATIKA MFUMO WA HOMONI
Tumeshaona kuwa, upungufu wa homoni
inayoitwa Testosterone inasababisha kukosa hamu ya kufanya tendo
la ndoa. Matatizo mengine katika mfumo wa homoni huchangia tatizo hili.
Kama Thyroid haitoi homoni za kutosha,
tatizo hili huweza kutokea ingawa mchango wa Thyroid katika tatizo hili
ni mdogo sana. Thyroid ni tezi ya kuzalisha homoni iliyopo katika eneo
la shingo.
UMRI MKUBWA
Kiwango cha Testosterone katika mwili wa
mwanaume hupungua kwa asilimia 1-2 kila mwaka kadiri anavyozidi kuwa na
umri mkubwa. Mara nyingi kuanzia miaka 50 na kuendelea. Homoni ya
msingi sana kuhusiana na masuala ya mapenzi huitwa Testosterone. Kwa
mwanaume homoni hii hutolewa kwa kiwango kikubwa na korodani na kwa
mwanamke hutolewa na Ovari.
Homoni ikipungua katika mwili wa
binadamu, humfanya apoteze hamu ya kufanya tendo la ndoa. Kiwango cha
Testosterone kikishuka sana katika mwili wa mwanaume huyu humfanya asiwe
na nguvu, ashindwe kutuliza mawazo kwenye jambo alifanyalo na apoteze
hamu ya kufanya mapenzi.
UCHOVU
Wakati mwingine uchovu husababisha
mwanaume kukosa hamu ya kushiriki tendo la ndoa. Na ikiwa mwanaume
atasongwa na shughuli nyingi zinazochosha mwili, hamu ya kushiriki tendo
la ndoa huanza kupungua na ikizidi, baadaye mwanaume atakosa kabisa
hamu ya kushiriki tendo na atahitaji uangalizi mkubwa ili arejee katika
hali ya kawaida.
Vilevile kukosa mpango mzuri wa shughuli
zako za kila siku na kujaribu kulazimisha kufanya mapenzi katikati ya
ratiba yako iliyojaa huchangia kukosa hamu ya kufanya tendo.
MSONGO
Msongo ni ugonjwa wa hali ya kuwa na
mawazo makali ya muda mrefu ya kukukosesha raha hali inayosababisha
kushindwa kuyafanya mambo yako ya kawaida kiufanisi. Mawazo ya namna
hii huathiri mwenendo wako wa maisha pamoja na matamanio yako
ya kimapenzi. Itaendelea wiki ijayo.
0 comments:
Post a Comment