Naibu Kamishna wa Uhamiaji Dar es Salaam, John Msumule jana alisema watuhumiwa hao wanatoka katika nchi 15.
Nchi hizo na idadi ya wahamiaji haramu ni Nigeria (4), China (20), Ethiopia (23), Korea (9), Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC (6), Somalia (3),Uganda (2), Madagascar (5), Burundi (2), Ivory Coast (1), Lebanon (1), India (1), Zimbabwe (1) na Ghana (1).
Alisema katika ‘kamata kamata’ hiyo pia wamefanikiwa kukamata Watanzania watatu, ambao wamekuwa wakijishughulisha na kukusanya, kuwahifadhi na kuwasafirisha wasichana kuwapeleka nchi za mbali, kwa ajili ya kufanya kazi mbalimbali.
“Tumewakamata wasichana sita ambao walikuwa wamekusanywa na watanzania hao ili kusafirishwa na tutawachukulia hatua za kisheria ili kutoa fundisho kwa wengine wenye nia ya kufanya mtindo kama huu,” alisema Msumule.
Msumule aliwataka wamiliki wa nyumba za kulala wageni na nyumba za kupanga, wahakikishe wanatambua wateja wao ni raia wa wapi na anafanya kazi gani, kabla ya kufanya naye mkataba wa aina yoyote.
Aliwataka pia watanzania wanaooa na kuolewa, wahakikishe wanafahamiana na mtu huyo na kumchunguza kujua anakotoka na yupo nchini kwa kazi gani, la sivyo mtu akibainika anaishi na mhamiaji, anaweza kujiingiza katika matatizo.
“Sisi hatutajali, tutamkamata kwa kosa la kumhifadhi kwa hiyo lazima wajenge dhana ya kuwachunguza watu hao, hata wasichana wa kazi za ndani, lazima umjue vizuri na sio unamchukua tu bila kujua historia yake ,” alisema.
Msumule aliwataka raia wengine ambao hawana vibali vya kuishi nchini, waondoke wenyewe na wasisubiri hadi sheria ichukue mkondo wake.
“Wapo wengi, tunachoomba waondoke wenyewe bila kushurutishwa, wengine wanafanya kazi ambazo hata watanzania wanaweza kuzifanya, wakubali na waondoke,” aliagiza.
0 comments:
Post a Comment