Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa, ilisema Mkapa alitoa kauli hiyo baada ya kukutana na kufanya mazungumzo Ikulu na Rais Magufuli.
Ilisema lengo la Mkapa kukutana na Rais Magufuli ni kumpongeza kwa dhamana aliyopewa na Watanzania kuiongoza nchi, kuunda Serikali na kumtakia heri ya mwaka mpya.
“Mkapa amemhakikishia Rais Magufuli kuwa yupo tayari kutoa ushirikiano wakati wote ama kufanya kazi yoyote endapo atahitajika kufanya hivyo,” ilisema taarifa hiyo.
Pia Rais Magufuli alikutana na Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba ambaye alisema Watanzania wote wanapaswa kumuunga mkono kiongozi huyo kwa kazi kubwa anazofanya ambazo ni kukomesha rushwa, ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka na wizi wa mali za umma.
Pamoja na kumtakia heri ya mwaka mpya, Jaji Warioba alimpongeza Rais Magufuli kwa jinsi alivyoanza kazi vizuri, hususani katika kusimamia ukusanyaji wa mapato, kubana matumizi na kuelekeza matumizi kwenye maeneo muhimu ambayo yanawahusu wananchi ikiwamo afya na maji.
Kauli ya Mkapa na Jaji Warioba imekuja siku moja tu baada ya juzi Rais mstaafu Jakaya Kikwete kumtembelea Rais Magufuli Ikulu na kufanya naye mazungumzo ambayo hata hivyo yameendelea kuwa ni siri.
Hii ni mara ya kwanza kwa viongozi wastaafu ndani ya siku mbili kumtembelea Rais Magufuli tangu ameingia Ikulu Novemba 5, mwaka jana.
0 comments:
Post a Comment