Chanzo kutoka ndani ya Nemc kimesema kuwa Suguti ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Sheria katika baraza hilo, alianguka ofisini kwake majira ya saa 9:30 alasiri baada ya kurejea kutoka katika Mahakama Kuu kitengo cha ardhi kushughulikia kesi inayoikabili Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi dhidi ya wakazi 681 wa eneo la Mkwajuni, Kinondoni ambao wanapinga nyumba zao kubomolewa.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa baada ya Suguti kuanguka ghafla ofisini kwake eneo la Mikocheni, baadhi ya wafanyakazi wenzake (wa Nemc) walimsaidia haraka kwa kumbeba na kumpakiza kwenye gari na kumpeleka hospitali mbili tofauti ambako kote vipimo vya awali havikubaini tatizo.
“Baadaye alipelekwa katika Hospitali ya Aga Khan ambako alilazwa kuanzia siku hiyo (Jumanne) na kutolewa leo asubuhi (jana) baada ya kupata nafuu… ila kwa kifupi ni kwamba afya yake imeyumba na hadi sasa madaktari bado wanachunguza kujua ni kitu gani hasa kinachomsumbua,” chanzo kiliiambia Nipashe jana.
“Nadhani ni uchovu ndiyo uliokuwa unamsumbua… hata hivyo, hayo ni masuala binafsi. "
Alipotafutwa kwa njia ya simu jana mchana, Suguti aliyekuwa akizungumza kwa taabu, alikiri kupatwa na tatizo asilolifahamu na kuanguka ofisini kabla ya kujikuta akiwa amelazwa katika wodi mojawapo ya Hospitali ya Aga Khan.
“Kwakweli sielewi kilichotokea. Nilipoingia ofisini kwangu baada ya kutoka kwenye kesi ya nyumba za watu wa Kinondoni, ghafla nikahisi kizunguzungu, giza kutanda na mwishowe nikaanguka… sijui kilichotokea baada ya hapo ila fahamu ziliponirudia nikajikuta nikiwa hospitali,” alisema Suguti.
Alipotakiwa kueleza zaidi kuhusiana na tukio hilo, Suguti hakuwa tayari kwa maelezo kuwa bado hajisikii vizuri.
“Kwa sasa naomba uniache tu, sijisikii kuzungumza zaidi,” alisema na kukata simu.
Zaidi ya nyumba 16,000 zimeshawekwa alama ya X katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam ambazo zinatakiwa kubomolewa kutokana na kujengwa maeneo hatarishi.
0 comments:
Post a Comment