MAJUTO MJUKUU! Umeshajua Unapendwa, Unatikisa Kiberiti Ili Iweje?

MUNGU ni mwaminifu kila wakati. Ametupa pumzi ya bure, mimi na wewe tunajidai kuuona Mwaka Mpya 2016. Yatupasa kumshukuru yeye ili azidi kutupa zaidi neema zake na hatimaye tuuone na mwaka ujao wa 2017.

Ni Jumamosi nyingine nakutana nanyi wasomaji wa safu yetu hii maridhawa. Kama kawaida hapa ni kupeana somo jipya la uhusiano kila wiki. Kama tulivyojifunza wiki iliyopita kuhusu suala la kuchungana katika uhusiano, wiki hii tunajifunza kuhusu somo lililopo hapo juu.

Kwa tuliokuwa pamoja wiki iliyopita nilisema, hakuna haja ya wapendanao kuchungana kama mbuzi. Nilieleza kwamba kila mtu anapaswa kujiheshimu na kuthamini penzi la mwenzake. Ajue kabisa anapochepuka anatengeneza maafa makubwa ya penzi lao pindi mwenzake atakapombaini.

Muhimu ni kuridhika na pale ulipo. Hakuna jipya, baki na mtu ambaye unaamini ni sahihi maishani mwako. Ukiwa mtu wa kujaribujaribu, utajipotezea muda na baadaye utakuja kuujutia.

Sasa turudi katika mada ya leo, kuna kawaida ambayo si rasmi imejijenga kwa mtu akishagundua anapendwa. Anajaribu kumtikisa mwenzake ili kupima tu ule upendo kutoka kwa mwenzake. Anajaribu kufanya jambo ambalo anajua kabisa hata haliwezekani katika hali ya kawaida, yeye atafanya tu ili aone utasemaje.

Tabia hii ipo kwa wanawake na wanaume lakini zaidi hufanya na wanawake. Mwanamke anakuwa anajua anapendwa, anatambua mpenzi au mume wake anampenda lakini anajaribu kumchokonoa ili kuona kama anapendwa kweli. Hiyo ndiyo furaha yake.

Mfano, anaweza kumuambi; ‘mbona kuna mtu kaniambia amekuona baa ukiwa na mwanamke.’ Anauliza swali hilo akiwa anajua kabisa si kweli. Anajua shughuli za mpenzi wake za kila siku namna ambavyo zinambana.

Hajakaa sawa, anajua mpenzi wake amechoka lakini badala ya kumpa pole ya kazi na kumfariji kwa namna inayofaa, anamuambia; ‘naomba ukanichotee maji bombani.’

Huo ni mfano tu. Mwanamke huyo anakuwa haumwi, mzima wa afya. Anatambua fika mpenzi wake amechoka kwa wakati huo lakini anamjaribu hivyo ili asikie atajibu nini.
Anaweza kujua kwamba mpenzi wake hapendi kitu fulani, kwa makusudi anakifanya hicho kitu ili kuona mpenzi wake atachukua hatua gani.

Hao ndiyo wanawake. Kwa upande wa wanaume pia wapo wa aina hiyo.
Akishagundua anapendwa, anaanza kutikisa kiberiti kwa kumjibu vibaya mpenzi wake. Anafanya vile akiamini kwamba kwa vile mpenzi wake anampenda sana, hawezi kufanya lolote. Analeta pozi tu makusudi moyoni akitoa kauli za ‘hapindui huyu…ameshakolea kwangu.’

Marafiki zangu, hapa lazima tujifunze kitu! Ukiona unapendwa sana na mwenzako, unapaswa kurejesha upendo kama au zaidi ya huo unaooneshwa na mwenzako. Unapaswa kuthamini penzi la mwenzako kwa hali na mali. Huna sababu ya kutikisa kiberiti, unaweza kufanya hivyo halafu ikawa ugomvi mkubwa utakaosababisha akuchukie kabisa.


Kumtikisa mwenzako siyo sifa. Umeshajua mwenzako anakupa upendo wa dhati, kwa nini na wewe usimuoneshe kama unampenda? Mapenzi ni hiari, kama mlikubaliana, mkapeana mikakati yenu, kwa nini msumbuane kwa vitu vya kipuuzi? Faida ya kuishi kwa amani na furaha katika uhusiano si ya mtu mmoja bali ni yenu wote.

Kama mmepanga safari ya kuelekea kwenye ndoa, hakuna haja ya kupimanapimana. Msichezeane hisia. Wewe mwenzako anakuwa ameshawekeza nguvu, akili na upendo wake, usimtafutie ‘visababu’ vya ajabu vitakavyosababisha ugomvi kila wakati.
Kwa leo ni hayo, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri ya kusisimua!
Share on Google Plus

About Anonymous

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment