Na Mwandishi Wetu, UWAZI
MWANZA: Bado Jiji la Mwanza limegubikwa na sintofahamu ya Polisi PC Daudi Elisha mwenye namba H 852 kumuua kwa kumpiga risasi askari mwenzake, PC Petro Matiko mwenye namba H 5990 kisha naye kujiua, mapya yameibuka.
Tukio hilo lililoitingisha Mwanza lilijiri saa 8 mchana wa Desemba 23, mwaka huu nje ya Benki ya Posta Tawi la Pamba.
Akizungumza na gazeti hili, kijana mmoja ambaye anadai alikuwa na
ukaribu na PC Elisha, huku akiomba hifadhi ya jina lake, alisema
anachokijua yeye kuhusu kisa cha mauaji hayo ni zaidi ya mchezo wa
upatu.
“Nilimuuliza ni kitu gani, akasema ni sapraizi. Hakuniambia ataua.
Kwa vile nilikuwa najua wanacheza upatu, sikupeleka mawazo kwamba
sapraizi hiyo ni kumuua mwenzake.
“Kuhusu sababu ya upatu, inaweza kuwa kweli lakini nijuavyo mimi,
Elisha alikuwa na ukaribu na dada mmoja anaitwa Jema lakini huyo dada
pia alikuwa na mazoea na Matiko. Elisha amekuwa akimtaka Matiko kuacha
mazoea na dada huyo lakini bila kuweka wazi kama yeye ni mpenzi wake au
la!
“Siku hiyohiyo, jioni yake, Elisha alimtuma mtu kwenda kwa Matiko
akimtaka amlipe pesa zake alizomkopesha kiasi cha shilingi laki mbili
(200,000) na alimpa masaa matatu tu. Lakini inaonekana Matiko aliamini
pesa hizo siyo sababu ya Elisha kumpa masaa matatu, bali kisa kinatokana
na ukaribu na huyo dada.
“Na yeye alimrudishia ujumbe kwa mtu huyohuyo akimwambia Elisha
kwamba, kama anadai kwa masharti hatamlipa lakini kama anadai
kistaarabu, atazipata na si kwa masaa matatu, bali kesho yake akienda
benki,” alisema kijana huyo.
Akaendelea: “Sasa nilipokuja kusikia kwamba, Elisha amempiga risasi
Matiko mpaka amefariki dunia naye kajiua, nilishtuka sana. Nikakumbuka
ile sapraizi aliyoniambia Elisha. Kwa hiyo naamini kama ni kumuua
Matiko, Elisha alishapanga muda, halikuwa wazo la ghafla.
“Matiko alisema hata asipokwenda benki, kama siku hiyo ni ya kupata
ajali, ataipata popote, hata akiwa amelala chumbani,” alisema kijana
huyo.
TUJIKUMBUSHE
Siku ya tukio, afande Matiko alifika kwenye benki hiyo akiwa kavaa
kiraia kwa lengo la kuchukua fedha. Lakini baada ya muda alitoka na
kuwaambia maafande waliokuwepo kwenye lindo ambao ni Elisha na PC
Remigius Alphonce (H 4291) kwamba, ameshindwa kutoa fedha kutokana na
mtandao kuwa chini.
Ilikuwa kufumba na kufumbua, Elisha alimfyatulia risasi Matiko.
Iliingia begani na kutokea mgongoni. Na yeye alijifyatulia chini ya
kidevu na kutokea kisogoni. Alifariki dunia palepale huku Matiko akifia
Hospitali ya Bugando.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, ACP Justus Kamugisha alithibitisha
kutokea kwa tukio hilo na kusema chanzo hakijajulikana huku jeshi la
polisi likiendelea na uchunguzi.
Mwili wa PC Matiko ulisafirishwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenda
kwao mkoani Mara kwa mazishi na mwili wa Elisha ulisafirishwa kwenda
Bariadi, Simiyu kwa mazishi.
0 comments:
Post a Comment