Huu Ndio Ukweli: Kubembelezwa Sana Siyo Kupendwa!

Hatuna budi kumshukuru mwenyezi Mungu kwa rehema na neema zake kutukutanisha tena Jumatatu hii katika kilinge chetu hiki cha XXlove kuzungumza yanayotusibu katika uhusiano wetu.
Baada ya kuzungumzia mada ya Mambo Yanayofurahisha Faragha kwa takriban wiki mbili mfululizo, leo tuangalie mada inayohusu baadhi ya wapenzi wanaobembelezwa na wenza wao na kuhisi kuwa wanapendwa sana kumbe wakati mwingine wanachezewa tu akili na hisia zao.

Simaanishi kuwa hustahili kubembelezwa au kubembeleza, la hasha, napenda ufahamu kuwa kuna aina mbili za kubembelezwa- kubembelezwa kiukweli na kubembelezwa kwa kulaghaiwa. Sehemu kubwa sana ya wanawake wamekuwa wakidanganywa kwa kubembelezwa sana na wao kujikuta wakiamini wanapobembelezwa ndipo penye penzi la kweli bila kung’amua kuwa wakati mwingine si kweli ni ulaghai wa hali ya juu unaofanywa na wapenzi wao.
Nitakupa mfano wa binti mmoja ambaye alikuwa na ushuhuda huu:

“Nilikuwa na mpenzi wangu, alinijali kila nilipokuwa na shida, hakusita kunisaidia kila nilipomuhitaji, alinipenda na nilimpenda ila baada ya muda nilimpata mpenzi mwingine ambaye alionekana kunijali sana na kunibembeleza muda wote na kunifanya nijisahau na nione kama yule wa mwanzo si mtu sahihi kwangu.
“Baada ya kunitumia, alinitelekeza na ndipo nilipogundua kuwa kumbe yule wa mwanzo alikuwa ana mapenzi ya kweli na ya dhati kwangu kuliko yule aliyejifanya ananibembeleza na kunipenda kinafiki.” Wakati dada akimalizia kuzungumza, alikuwa akijifuta machozi na kujutia kumpa nafasi mtu ambaye hakuwa na mapenzi ya kweli bali alitengeneza upendo wa uongo na kuvaa uhusika wa kubembeleza kumbe alikuwa tapeli mkubwa.

Ni kweli mapenzi yanahitaji mbembelezaji na mbembelezwaji lakini kiukweli kuna wanaume na wanawake wamejikuta wakiumia mno maishani mwao baada ya kugundua walibembelezwa kinafiki na wao kuwakabidhi mioyo yao waliowabembeleza na kuona wamefika.

Sina uhakika sana kama kubembelezwa ni kipimo cha penzi la dhati pamoja na kupendwa kiukweli, kwani kuna wengine hawajui kubembeleza sana ila wana mapenzi ya kweli kwa wenza wao.Kwa tabia hiyo ya kupenda kubembelezwa, wengi wamejikuta wakiangukia pua baada ya kutendwa na matapeli hao wa mapenzi.

Kuna kitu kikubwa sana cha kujifunza msomaji wa makala hii, kaa chini utafakari kuhusu kubembelezwa kwako kisha tuma maoni yako, nami nitayatoa wiki ijayo.
Pia usikose kutembelea ukurasa wetu wa Mimi Na Uhusiano kwenye Mtandao wa Facebook na WhatsApp kujifunza mengi kuhusu mapenzi.
Share on Google Plus

About Anonymous

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment